Thursday , 3rd Nov , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, Serikali imekwishapeleka zaidi ya sh. bilioni 177 kwenye halmashauri mbalimbali nchini ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

 

Ametoa kauli hiyo leo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Munde Tambwe aliyetaka kupata kauli ya serikali kuhusu ucheleweshwaji wa fedha za bajeti ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu amesema serikali ilianza kupeleka watumishi watakaosimamia ukusanyaji mapato katika halmashauri zote nchini. Kutathmini miradi yote iliyoanza ambayo haijaendelezwa pamoja na mipya ili kutambua thamani na kisha kupeleka fedha.

 Amezisisitiza halmashauri hizo kuendelea kukusanya mapato ndani ili kuongezea bajeti kwa fedha wanazopelekewa na watumie mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti mapato hayo.

Aidha, Waziri Mkuu amezitaka halmashauri zote nchini zihakikishe fedha zinazopelekwa katika maeneo yao zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa miradi husika.

Amewasihi Wabunge wafuatilie na wasimamie matumizi ya fedha hizo ili miradi iliyopangwa iweze kukamilika.