Tuesday , 4th Dec , 2018

Mbunge wa Jimbo la Bunda, Esther Bulaya amemjia juu Waziri Maliasili na Utalii, Dkt Hamis Kigwangala kwa kile alichokidai kuwa kiongozi huyo hakutumia busara wakati akilizungumzia suala la sheria mpya ya mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2018 kupitia mitandao ya kijamii.

Waziri Maliasili na Utalii, Dkt Hamis Kigwangala, Mbunge wa Jimbo la Bunda, Esther Bulaya.

Bulaya ametoa madai hayo wakati akizungumza na waandiishi wa habari Jijini Dar es salaam, juu ya sheria ambapo alidai kuna viongozi wenzake ambao ni vijana wamekuwa wakimuangusha kwa kuwa wana mamlaka.

"Nimesoma twiti za Kigwangala, mimi nasema yule ni mchumia tumbo anashindwa kutambua kuna wazee wamenifuata kulalamika hawajalipwa mafao kwa miaka 2, anataka tuamini kuwa yale ndiyo maoni ya Baraza la Mawaziri, asisahau hata yeye aliendesha mgomo wa madaktari alivyokuwa Daktari muhimbili," amesema Bulaya.

Wakati huo huo Bulaya amemshukuru Spika Job Ndugai kwa kile alichokieleza kuwa amempongeza juu ya msimamo wake kuhusu  suala ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Namshukuru Spika Ndugai kwa kunipongeza nimezipokea pongezi zake, lakini haiondoi ukweli kwamba chanzo cha tatizo hili ni wabunge wa CCM kutumia wingi wao vibaya kwa kuona yale maoni tunayotoa sisi ni maadui, lakini namshukuru ila kwenye moyo anajua walichokifanya," ameongeza.