Wednesday , 22nd Apr , 2015

Wanawake 255 kati ya wanawake 100,000 hupoteza maisha kila mwaka kwa ajili ya uzazi na huku wengi wakijifungulia majumbani kwa zaidi ya asilimia 60, na kusema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuifikisha elimu ya afya ya uzazi hadi mashuleni.

Wananchi wakifuatilia huduma ya vipeperushi vinavyoelezea huduma za uzazi wa mpango baada ya kuletewa na MARIE STOPES TANZANIA.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Shirika la Marie Stopes Bi Elly Reweta ameyasema hayo mjini Mpanda mkoani Katavi, wakati shirika hilo lilipokuwa likizindua rasmi huduma za uzazi wa mpango kwenye mkoa huo na kuongeza kuwa wasichana 8,000 hupoteza haki yao ya kupata elimu kwa kupata mimba zisizotarajiwa.

Jamii imekuwa haipati elimu ya afya ya uzazi kwa uhakika nchini, hali inayosababisha kiwango cha watu wengi walioko kwenye ndoa kushindwa kutumia uzazi wa mpango kupanda hadi asilimia 25 kutoka asilimia 23 ilivyokuwa awali.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mpanda Paza Mwamlima, akimwakilisha mkuu wa mkoa huo wa Katavi Dakta Ibrahim Msengi katika uzinduzi huo, ametoa wito kwa jamii ya mkoa huo wenye miaka minne tu tangu uanzishwe, kutumia kwa dhati huduma za uzazi wa mpango zinazotolewa na Marie Stopes.

Panza ameongeza kuwa elimu ya uzazi ndiyo suluhu ya kukabiliana na tatizo la vifo vingi vya akina mama na watoto wachanga, vinavyosababishwa na ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi kwenye maeneo mengi mkoani humo