Wednesday , 29th Jun , 2016

Watafiti kutoka Uingereza wamegundua hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi adimu zaidi ya Helium nchini Tanzania.

Moja ya mitambo ya kuchakata gesi iliyopo nchini Tanzania.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford na kile cha Durham kwa ushirikiano na wataalumu wa madini kutoka Norway wamegundua uwepo wa takriban futi bilioni 54 za gesi hiyo ya barafu kama inavyofahamika.

Ugunduzi huo umefanyika katika eneo la bonde la ufa la Tanzania.

Katika taarifa kwa wanahabari huko Japan, watafiti hao wanasema kuwa uhaba wa gesi hiyo kote duniani ulikuwa umesababisha taharuki haswa kwa madaktari ambao wanatumia gesi hiyo adimu kuendesha mashine za utabibu zijulikanazo kama MRI scanners, mbali na kutumika katika mitambo ya kinyuklia miongoni mwa sekta zingine nyingi za kawi na teknolojia.

Kabla ugunduzi huo watafiti walikuwa wamebashiri ukosefu wa gesi hiyo baridi ifikapo mwaka wa 2035.