Tuesday , 3rd May , 2016

Mahakama ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela mkazi mmoja wilayani humo Evaristo Msemwa(35) kutokana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kadhalika mahakama hiyo imemwachia huru mshitakiwa namba mbili katika shitaka hilo Kefa Ndekwa (40) baada ya mahakama kujiridhisha kuwa hana hatia.

Awali ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa polisi, Mazoya Ruchagura mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya ya Mbarali Alis Mkasera kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Oktoba 28 mwaka jana.

Ruchagura alisema mnamo majira ya saa tano usiku washitakiwa hao wawili walivamia nyumbani kwa mkazi wa kijiji cha Mkandawi wilayani Mbarali, Ashery Mpanyakavi wakiwa na mapanga na visu na kupora fedha taslimu shilingi milioni moja.

Alisema kabla ya kupora fedha hizo, watu hao walimjeruhi Mpanyakavi kwa kutumia silaha walizokuwa nazo ambapo walimng’oa meno mawili na kasha kuondoka wakitumia gari aina ya Toyota Chaser yenye namba za usajiri T 278 BMJ.

Hata hivyo baadhi ya wakazi kijijini hapo walistushwa na ujio wa watu hao walipobaini kuwa walikuwa wahalifu walipiga simu kijiji cha pili cha Kangaga na wakazi wa kijiji hicho wakafanikiwa kuwakamata na kisha kuwapeleka kituo cha polisi Rujewa.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo, hakimu mkazi Alis Mkasera alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote na kuwa mshitakiwa namba moja Evaristo Msemwa anapaswa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, kulipa shilingi milioni moja alizoiba na pia fidia ya shilingi laki nane kutokana na kumjeruhi mlalamikaji.

Kwa upande wa mshitakiwa namba mbili Kefa Ndekwa, alisema mahakama inamuachia huru kutokana na mlalamikaji kumtambua na kuithibitishia mahakama juu ya mshitakiwa namba moja pekee, hatua inayoonesha mshitakiwa wa pili hakuhusika na tukio hilo.