Saturday , 29th Dec , 2018

Waziri wa zamani wa kipindi cha Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere Pancras Ndejembi amefariki Dunia leo Desemba 29, 2018 katika Hospitali ya Rufaa Mkoani Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu dhidi ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Chama Cha Mapinduzi.

Mbali na nafasi hiyo nyeti Ndejembi pia alikuwa moja ya Makada wa Chama Cha Mapinduzi ambao walihudumu kwenye nafasi mbalimbali ikiwemo Ukuu wa Wilaya kwenye wilaya mbalimbali nchini pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mikoa wa Chama Cha Mapinduzi.

Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho mtoto wa kada huyo  Edna Ndejembi amesema "jana jioni hali yake ilibadilika ghafla ndipo tukamkimbiza hapo hospitali ya mkoa na leo saa tatu asubuhi mzee ametutoka,"

Ameongeza kuwa Mzee Ndejembi alikuwa anasumbuliwa na kifua kubana ambapo alilazwa katika Hospitali ya DCMC ya Jijini Dodoma na kuruhusiwa juzi Alhamisi akiwa ameimarika kiafya.

Miongoni mwa wabunge ambao wameonesha kuguswa na tukio la kifo cha Ndejembi ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ambapo ameandika "Mungu ailaze roho ya Mzee Ndejembi mahali pema peponi ni msiba mzito kwa familia ya Ndejembi lakini pia ni msiba kwa viongozi na vijana ambao walipata fursa ya kumfahamu Mzee Ndejembi."