.jpg?itok=Xpn8Uvop×tamp=1503848894)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu ametoa maombi hayo alipokutana na Makamu wa Rais wa Cuba, Bi. Gladys Bejarano ambapo ameimba Serikali hiyo iendelee kutoa ufadhili wa masomo kwa madaktari hao hadi ngazi ya shahada ya uzamili kwa sababu Serikali ya Tanzania inawahitaji madaktari bingwa wengi kwani walioko nchini ni wachache.
Pamoja na maombi hayo Mh. Majaliwa amemuahidi Makamu huyo wa Rais kuwa Tanzania itafungua ofisi za Ubalozi nchini humo huku akimuhakikishia kuwa taifa linaheshimu mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kiafya na kiutamaduni kati yake na Cuba.
“Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati Tanzania na Cuba, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere, hivyo lazima tufungue ofisi za ubalozi na tutamleta balozi wetu hapa.” Mhe. Majaliwa
Makamu huyo wa Rais alisema Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa Sekta za Afya, Utamaduni, Kilimo, Uchumi na Elimu. Kuhusu ombi la kuongeza ufadhili wa shahada ya uzamili kwa madaktari alisema amelipokea na atalifanyia kazi.
Kwa upande mwingine Bi. Gladys amemshukuru Waziri Mkuu kwa kufanya ziara nchini Cuba na kumhakikishia kuwa uhusiano kati ya Cuba na Tanzania utaendelea kuimarishwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Amesema serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha uchumi wake unakua kwa kasi jambo ambalo ni tofauti na mataifa mengine. “Nawapongeza kwa hatua za kimaendeleo mnazozifanya.”