Thursday , 20th Dec , 2018

Zikiwa zimesalia siku 11 Mwaka 2018 kufikia ukingoni, kwa baadhi ya watu ulionekana kuwa mrefu, na kwa wengine ukionekana kuwa mfupi kutokana na sababu mbalimbali kitu ambacho si rahisi kusahaulika kwa mwaka huu.

Mfanyabiashara Mohamed Dewji

Yapo matukio mbalimbali makubwa yasiyosahaulika ya kijamii, siasa, michezo yaliyotokea mwaka 2018 ambayo ni ya kuhuzunisha na mengine ya kufurahisha kama uzinduaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama 'Mfugale Flyover', barabara na miradi ya umeme. Matukio mengine ni ya utekaji, uhamaji wa vyama, Ajali za kutisha na mengineyo.

Tukio ambalo halitaweza kufutika vichwani mwa wa Tanzania wengi ni pamoja na ajali iliyotokea  Septemba 20, ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere katika kisiwa cha Ukara ndani ya Ziwa Victoria, wilayani Ukerewe na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 220.

Baada ya ajali hiyo, Mbunge wa Ukerewe, Joseph Michael Mkundi alitangaza kuhamia CCM kwa madai kwamba Chama chake cha zamani (CHADEMA) kupoteza heshima na utu baada ya kumtelekeza katika kipindi ambacho alihitaji msaada na ushirikiano kutoka kwenye chama hicho na uongozi wake.

Tukio lingine ambalo haliwezi kufutika kirahisi kwenye vichwa vya watanzani ni lile la Mfanyabiashara maarufu nchini na Tajiri kijana namba moja barani Afrika, Mohammed Dewji 'Mo' kutekwa majira ya saa 11 Alfajiri nje ya hoteli ya Colosseum alipokuwa akienda kwenye mazoezi.

Kutekwa kwa Mo hakukuitikisa Tanzania pekee kwani vyombo vikubwa vya habari ulimwenguni viliripoti na kufuatilia kwa ukaribu, huku taarifa za awali zikidai kwamba waliotekeleza tukio hilo walikuwa wageni kutoka nje ya Tanzania.

Hata hivyo baada ya siku tisa, Mo alipatikana huku Polisi wakiahidi kula sahani moja na watekaji na Mkuu wa jeshi la Polisi , Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro akisema  kuachiwa kwa Mo ni mwanzo wa kuwanasa wahalifu hao.

Waraka wa Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na ule wa KKKT ambao ulionya kuhusu matukio ya watu kutekwa, kupotea, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi viliamsha taharuki kila kona ikiwepo kwenye mitadao ya kijamii ambapo ilipelekea viongozi wakubwa serikali kutoa majibu.

Hata hivyo Waraka huo ulipelekea kusambaa kwa barua kutoka  kwa Mkurugenzi wa Usajili wa Vyama vya Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba alipowaandikia TEC na KKKT akitaka wajieleze huku aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliikana barua hiyo. Siku chache baadaye Rais Magufuli alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri huku Mwigulu akiwekwa kando.

Wakulima wa zao la Korosho mwaka 2018 hawatausahau baada ya kugomea kuuza korosho kwenye minada kwa kile walichokiita bei kuwa ndogo, Serikali ya Tanzania iliamua kujitosa kwa ajili ya kumkomboa mkulima ambapo badala ya kununua kwa bei elekezi ya sh. 3000, yenyewe ilinunua kwa Sh. 3300.

Hata hivyo tofauti na serikali kuingilia kati biashara ya zao la korosho, serikali iliagiza jeshi kuhakikisha inashugulikia biashara hiyo mpaka mwisho katika suala la usafirishaji.

Matukio mengine ambayo Watanzania hawatayasahau mpaka pale yatakapopatiwa ufumbuzi ni kama mjadala malipo ya ya watumishi, Viongozi wa upinzani kutumia muda mwingi mahakamani, Wabunge na madiwani wa upinzani kuhamia chama tawala na nchi za Ulaya na Marekani kuizungumzia demokrasia ya Tanzania.