Wednesday , 14th Dec , 2016

Tathmini ya afya iliyofanyika mwaka 2015 ya mpango wa matokeo makubwa sasa inaonesha mikoa ya kanda ya ziwa inaongoza kuwa na viashiria hafifu vya afya ya mama na mtoto sambamba na ukosefu wa damu salama.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akikabidhi gari la wagonjwa kwa wabunge a mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati akipokea msaada wa magari 50 ya kubebea wagonjwa na magari 8 kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto kutoka WHO na Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), magari ambayo yatatumika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema sababu kubwa inayochangia vifo vya akina mama wajawazito na watoto ni huduma mbovu za hospitali za rufaa ambazo huchangiwa na miundombinu mibovu ambayo hukwamisha wagonjwa kupata kukimbizwa hospitali kwa haraka.

Amesema Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha katika kipindi cha miaka 20 iliyopita Tanzania imeweza kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto kutoka vifo 580 katika kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 482 kwa sasa.

Kwa upande wao wawakilishi wa wananchi wa mikoa hiyo ya kanda ya ziwa ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesema ni vyema kina mama waendelee kupewa elimu ya uzazi ili kuwakinga na vifo na vilema ambavyo kama havitadhibitiwa kwa haraka vinaweza kusababisha maafa makubwa kwa taifa.