Wednesday , 31st May , 2017

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo  la Moshi Mjini na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kilimanjaro,Mzee Philemone Ndesamburo amefariki asubuhi leo

Mzee Philemon Ndesamburo (enzi za uhai wake)

Taarifa za awali kutoka kwa Afisa Habari wa CHADEMA zimeeleza kuwa Mzee Ndesamburo ambaye pia ni muasisi wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini amefariki dunia katika Hospitali ya KCMC, Mkoani Kilimanjaro baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa hospitalini hapo

Mzee Ndesamburo mbali ya kuwa mwanasiasa na mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15 hadi mwaka 2015, pia alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa katika sekta ya utalii na mmiliki wa hoteli mbalimbali katika Kanda ya Kaskazini.

Kazi ya mwisho kuifanya katika maisha yake ni kusaini cheki ya rambirambi ya wafiwa wa watoto 32, waalimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki katika ajali mwanzoni mwa Mei mwaka huu.

Akizungumza kwa masikitiko kwa njia ya simu ya kiganjani, leo  Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema kuwa amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho.

Golugwa amesema Jumamosi alikuwa naye Dodoma na akapiga  naye picha, lakini alimuahidi leo amfuate Moshi ampe rambirami ya wafiwa wa ajali ya shule ya Luky Vicent,lakini jana alimpigia simu akaomba akachukue rambirambi hiyo leo na akamtuma Meya wa Jiji la Arusha Calist Lazaro na aliingia ofisini wakati anasaini cheki akasikia vibaya na kukimbizwa hospitali ya Rufaa KCMC.

Golugwa amesema wakati akisaini cheki hiyo  ya Sh.milioni 3.5  alikuwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye ilikuwa akabidhiwe cheki hiyo ili ailete kwa wafiwa Arusha.

Amesema ngumu kuamini kifo kimetokea ghafla , maana kakimbizwa hospitali KCMC na kuambiwa amefariki, sasa wanasubiriwa watoto wake ili kuufanyia uchunguzi mwili wake,kutokana na mazingira ya kifo kilivyotokea.

Amesema baada ya hapo Chama kitatoa taarifa rasmi ya kuondokewa na mkongwe huyo katika chama,baada ya kuwasiliana na wanafamiliya na wengine. Golugwa amesema wakati hali hiyo ilipomkuta katika ofisi yake ya Keys Hotel, alikimbizwa hospitalini na  dereva wake, mtoto wake mmoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Calist Lazaro