Wednesday , 19th Dec , 2018

Mkoa wa Kagera umetakiwa kujenga vyumba vya madarasa 351 ili kuwezesha wanafunzi zaidi ya 14,000 ambao wamemaliza darasa la saba mwaka huu na kufaulu, kukosa nafasi za kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza, ili kuhakikisha wote wanapatiwa nafasi.

Wanafunzi wakiwa wamekusanyika.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa elimu ambacho mbali na shughuli nyingine kimeweka mikakati itakayowezesha wanafunzi hao kupata nafasi za kuendelea na masomo, afisa elimu wa mkoa wa Kagera Aloyce Kamamba amesema kuwa kati ya wanafunzi 39,545 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, wanafunzi 25,499 ndiyo waliochaguliwa.

Wakizungumza katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe wameshauri wazazi wenye watoto waliofaulu kuitwa na kuelezwa mipango iliyopo, na jamii nzima ya Wanakagera waishio ndani na nje ya mkoa kuhamasishwa kutoa michango kwa ajili ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa, badala ya kutegemea serikali pekee.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Marco Gaguti amewataka wajumbe hao kuweka mikakati itakayowezesha kupunguza tatizo la uhaba wa madarasa kwa waanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza