
Nape Nnauye
Akizungumza leo katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani, ambao kitaifa umefanyika jijini Mwanza, Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Nape Nnauye, amesema kufuatia sheria ya magazeti ya 1976 kuonekana ni miongoni mwa sheria kandamizi kwa uhuru wa habari, lazima wadau hao waweze kuunda ‘timu’ ambayo itaenda mjini Dodoma kuonana na waziri na waandishi wa Bunge.
Amesema sheria hiyo ni moja ya chanzo cha kusimamisha matangazo ya moja kwa moja Bungeni.
“Nakubaliana na hiyo changamoto, lakini napenda kuwashauri muunde timu ya watu kadhaa ili mje Bungeni Dodoma kuonana nasi, warusha matangazo wa Bunge na kutembelea studio yenyewe, kisha tuzungumze,” alisema Nape.
Nape amesema serikali itakaa chini ili kuona sheria zinazokwaza vyombo vya habari zinafanyiwa kazi: Kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho hayo ni, kupata taarifa ni haki yako ya msingi, idai.
Alisema lazima yakusanywe maoni na kufikishwa Bungeni ili yaweze kufanyiwa kazi mawazo ya wadau wote ili kutopuuzwa na wazo lolote, lengo ni kutaka kuona uhuru wa vyombo vya habari unafanikiwa.
“Tukosoe bila uoga ili tuweze kusonga mbele kwani serikali na wadau wa habari si maadui,” alisema.
MWENYEKITI MOAT
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (Moat), Dk. Reginald Mengi, amesema ili vyombo vya habari viweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu, lazima serikali itoe uhuru wa kupata habari.
Dk. Mengi amesema vyombo vya habari haviwezi kutimiza wajibu wao kwa weledi kama watumishi wa umma watakataa au kughairi kutoa habari kwa visingizio vyovyote, hasa kwa madai ni siri ambazo hazipaswi kuchapishwa kwa usalama wa taifa.
Aidha, Dk. Mengi amewataka waandishi wa habari kuandika habari za kimaendeleo na kuchochea uchumi wa nchi pamoja na kufahamu changamoto husika na jinsi ambavyo zinaweza kutatuliwa.
Amesema vyombo vya habari si adui wa jamii bali ni kioo cha jamii, hivyo lengo kubwa ni kuandika habari za ukweli na zile za furaha kwa jamii kuliko kuandaa za huzuni kila siku.
Pia, Dk. Mengi amesema vyombo vya habari vinatakiwa kujikita zaidi kuandika habari za mauaji ya albino na ujangili, lakini alishauri kufuatilia kwa undani watu wanaowatuma wauaji wa watu hao na tembo ili sharia iweze kuwabana.
MWENYEKITI WA MISA-TAN
Awali Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa TAN), Simon Berege, aliiomba serikali kufuta uamuzi wake wa kuzuia urushwaji wa matangazo ya Bunge ya moja kwa moja kutokana na kutokuwa na tija kwa Taifa.
Alisema sheria hizo ni namna nyingine ya kuminya haki ya wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati kutoka kwa wawakilishi wao.
MGENI RASMI
Jaji Mkuu wa Tanzania, Chande Othman, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza, Robert Makaramba, amesema uwepo wa sheria nzuri za vyombo vya habari na upatikanaji wa taarifa ni chachu kubwa ya maendeleo nchini.
Jaji Makaramba alisema sheria hizo haziwezi kupatikana bila ya ushirikishwaji wa kina wa wadau husika na kutoa angalizo kwa serikali kuacha kung’ang’ania sheria zisizo rafiki kwa vyombo vya habari ili kuinua uhuru wa vyombo vya habari kidunia.
Hadi kufikia mwishoni mwa Aprili mwaka huu, Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya 71 ya viwango vya uhuru wa vyombo vya habari kati ya nchi 180 duniani ambazo zimefanyiwa utafiti na taasisi ya wanahabari wasio na mipaka.
Siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani huadhimishwa Mei 3, kila mwaka, duniani kote kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1993, maadhimisho ya mwaka huu ni ya 25 tangu kuanzishwa kwake na azimio la Windhoek la kanuni ya uhuru wa habari.
