
Wakili James Mrenga akiongea na EATV katika mahojiano maalum jijini Dar es salaam, amesema, kutenda kosa la jinai hakuondoi haki za mtoto kupewa stahiki zake, hivyo kuitaka serikali kuhakikisha inakuwa na mahakama za watoto, iongeza shule za maadilisho na kuweka mazingira rafiki kwa watoto kuanzia ngazi ya polisi na mahabusu za kuwahifadhi watoto kulingana na mahitaji yao.
“Mara nyingi watoto wanajumuishwa kwenye Mahakama na magereza za watu wazima, jambo hili ni kinyume na hadhi za mtoto, ni kinyume na mkataba wa kimataifa wa mtoto ambao Tanzania kama nchi imeridhia ambao unajulikana kama “Juvenile Justice” (United Nation Covention on the Right and Welfare of the Children. CRC)
James Mrenga amesema bado mahakama zetu hazijawakumbuka watoto, huku idadi kubwa ya mahakimu wakiwa hawana mafunzo ya kutosha kuendesha kesi za watoto, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kunyima haki watoto na kushindwa kujitetea.
Mkufunzi wa haki za watoto Bi. Pili Mtambalike amesema ni lazima serikali iwakumbuke watoto kwa kutenga rasilimali za kutosha kwa maafisa ustawi ili kuongeza juhudu za kuwalinda watoto katika ngazi ya mtaa na vijiji hasa wanaoshikiliwa na vyombo vya sheria na kutelekezwa na wazazi wao.
“Wengi wa watoto wa namna hii ni matokeo ya malezi mabovu ya familia, wengine baada ya kufiwa na wazazi au wazazi wanapotengana wanaingia kwenye wakati mgumu na kupelekea kukosa malezi bora na baadaye wanajiingiza kwenye uhalifu kwa lengo la kujitetea na hali ngumu walionayo. Matokeo yake tunawaita wahalifu na kuwatenga, kutokana na matokeo ya maisha wanayopitia, hivyo kuwatetea ni wajibu wetu” amesema.
Wanaharakati wanaelezea kuwa watoto wanaweza kujikuta kwenye mgogoro na sheria kwa kushirikishwa kutenda makosa ya jinai, kufundishwa matumizi ya silaha na wizi, kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo malezi na mambo mengine mengi.
