Sunday , 21st Feb , 2016

Mgombea kiti cha urais wa chama cha Republican katika uchaguzi ujao wa urais nchini Marekani Donald Trump ameshinda kura za maoni katika jimbo la South Carolina.

Bwana Trump ambaye awali mwezi huu, alishinda katika jimbo la New Hampshire, amepata kura nyingi katika jimbo hilo na kuwabwaga wapinzani wake Ted Cruz na Marco Rubio wakimfuatia ambao wamekuwa wakimfuata kwa karibu.

Trump amepata asilimia 32.50 ya kura zote akifuatiwa na Rubio aliyepata asilimia 22.48, huku Ted Cruz akiwa na asilimia 22.32.

Katika hatua nyingine, gavana wa zamani wa Florida, Jeb Bush, ambaye ni kaka wa aliyekuwa Rais wa Marekani George W. Bush, amejiondoa katika kinyanganyiro hicho, kutokana na matokeo mabaya.

Bush ameshika nafasi ya 4 baada ya kupata asilimia 7.84 ya kura zote katika jimbo hilo la South Carolina.

Kwa upande wa chama cha Demeceatic, Bi Hillary Clinton ameibuka mshindi jimbo la Nevada, na kumbwaga mpinzani wake wa karibu, Bernie Sanders.