Friday , 15th Jan , 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watanzania kujikita katika kuimarisha miundombinu ili kukuza uchumi, kwani kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji ni muhimu kwa shughuli mbalimbali mfano kilimo na biashara.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ardhi , Miundombinu, Uchukuzi, na Utalii wa Japan, Bw. Takatoshi Nishiwaki

Akizungumza na wadau wakati akifungua mkutano wa miradi ya ubia katika ujenzi wa miundombinu kati ya Tanzania na Japan (TANZANIA -JAPAN PUBLIC -PRIVATE QUALITY INFRASTRURE CONFERENCE) uliofanyika leo, katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam, amesema sekta binafsi inasaidia katika ujenzi wa miundombinu na sekta ya usafirishaji kwa ujumla, ambapo ni muhimu kwa vile inasaidia kuboresha maisha ya watu.

“Serikali kupitia Kituo cha uwekezaji nchini (TIC) imeandaa mazingira mazuri ya biashara inayosaidia wawekezaji kuja kuwekeza nchi, matumaini yetu ni kwamba kutokana na mkutano huu wawekezaji wa ndani mtapata fursa ya kujifunza na kujiunga katika kampuni ambazo zitawasaidia kushirikiana na kampuni za kijapani na kuweza kupata ujuzi, utaalamu wa kiutawala na uwezo wa kuwa wabunifu zaidi hasa katika masuala ya miundombinu.” amesema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea kwa kusema kuwa mkutano huo utaimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japani, na kutoa fursa ya kubadilishana ujuzi kwa wakandarasi, washauri, kampuni za biashara na uhandisi kutoka Japani na Tanzania, vilevile utawawezesha kujenga mtandao kwa kushirikiana na makampuni ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wa miundombinu na usafirishaji, Tanzania ina ukubwa wa barabara zinazofikia kilomita 87,581, kutokana na sera na jitihada mbalimbali kwa kipindi cha miaka 10 (2005-2015) jumla ya kilomita 17,762 zimefikia hatua mbalimbali za ujenzi.

Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema, Tanzania ina mifumo miwili ya reli, reli ya kati yenye kilomita 2,706 na reli ya ‘Tanzania Zambia Railway Authority’ (TAZARA) yenye kilomita 975. Pia, ina Bandari kuu za Dar es salaam, Tanga na Mtwara .

Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa (National ICT Broadband Backbone -NICTBB) kwa kutumia mfumo wa baharini (SEACOM, July 2009) na (EASSY April, 2010) tayari nchi jirani za Rwanda, Zambia na Kenya zimeunganishwa na mkongo huo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani, amesema miundombinu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi yeyote ile duniani. Tanzania na Japani zimeshirikiana katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali, mfano barabara za Dodoma –Iringa, Namtumbo –Tunduru, Dodoma – Babati inayoendelea kujengwa, upanuzi wa barabara ya Gerezani pamoja na ‘fly over’ ya TAZARA.

Naye, Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japani Takatoshi Nishiwake amesema, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alipotembelelea Japani alisema angependa kuona Japani na Tanzania zinashirikiana katika masuala ya ujenzi wa miundombinu.

Ameendelea kwa kusema kuwa, serikali ya Japani inapenda kubadilishana ujuzi na Tanzania katika masuala ya miundombinu, pia ni matumaini yake kuwa washiriki kutoka pande zote mbili wanapata fursa ya kubadilishana ujuzi na kujifunza zaidi. Vile vile kupitia mkutano huu mahusiano ya nchi hizi mbili yataimarika zaidi.