Wednesday , 2nd Nov , 2016

Takwimu za kidunia zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 2016 takribani waandishi wa habari 1,300 wamepoteza maisha wakiwa katika kazi zao mbalimbali za kiuandishi.

Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa.

Kitaifa takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka waandishi wa habari 30 wanaripotiwa kupatwa na majanga wakati wakitimiza wajibu wao wa kutafuta na kutoa habari.

Takwimu hizo zimetolewa na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Ole Ngurumwa kwenye mkutano wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupambana na kuzuia ukatili kwa waandishi wa habari duniani.

Amesema ni wakati sasa jamii na serikali ihakikishe inasimamia ulinzi na kutetea haki za waandishi wa habari kulingana na makubaliano mbalimbali ya kimataifa.

Kwa upande wake mwakilishi wa serikali na Kaimu Mkurugenzi Habari Maelezo katika Mkutano huo Bw. Jamal Zuberi amesema tayari serikali imeanza kusikiliza kesi mbalimbali ambazo zinawagusa waandishi wa habari kwa kuwanyima haki zao.