Friday , 7th Oct , 2016

Jumuiya ya Wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameahidi kupitisha mizigo yao katika bandari ya DSM kutokana na kuridhishwa na utendaji wa bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kudhibitiwa kwa vitendo vya wizi na upotevu wa mizigo.

Bw. Sumaili Edward

Rais wa Wafanyabiashara hao Bw. Sumaili Edward, ametoa ahadi hiyo leo Jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache tu kupita tangu Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila kumaliza ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine aliahidi kuendelea kutumia bandari za hapa nchini kwa mizigo yote inayokwenda na kutoka nchini mwake.

Katika mkutano wake na wanahabari, Bw. Sumaili amekwenda mbali na kusema kuwa wamefurahishwa na ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kutoa muda wa nyongeza kwa mizigo ya Kongo, sambamba na hatua za haraka za kuwafidia wafanyabiashara wa nchi hiyo ambao mizigo na shehena zao ziliuzwa na kupigwa mnada kimakosa.