Tuesday , 11th Oct , 2016

Wanafunzi wa shule ya msingi Nakatete, iliyopo halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wanalazimika kusomea chini ya miti ya mikorosho kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa unaikabili shule hiyo.

Picha (Maktaba)

Wakizungumza na East Africa Radio, wanafunzi wa darasa la tano Mrani Jamal na Asha Masoud, wamesema kuwa hali hiyo inawafanya waathirike zaidi kipindi cha mvua, jua kali na kukosa wigo mpana wa kujifunza kutokana na udogo wa mbao za kujifunzia.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Naipha Mtongwechi amesema jamii ya kijiji hicho haina mwamko katika elimu hali ambayo inapelekea watoto kutoona umuhimu wa kujiunga na elimu ya sekondari na kwamba toka kuanza kwa shule hiyo mwaka 2005 ni mwanafunzi mmoja pekee aliyemaliza kidato cha Nne.

Katika kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa, mkuu wa wilaya ya Nanyumbu Joachim Wangabo amekabidhi mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya kuanza ujenzi wa madarasa huku wadau wengine wakitoa michango ya pesa na vifaa.

Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2005 pia inakabiliwa na uhaba wa walimu, nyumba za walimu pamoja na ukosefu wa matundu ya vyoo.