Saturday , 25th Jul , 2015

Wanasiasa wanawake nchini wametakiwa kudumisha amani wakati wa kufanya kampeni zao za uchaguzi ili kuiepusha nchi na machafuko yanayotokana na uchaguzi mkuu.

WANAWAKE wakiwa katika maandamano kwenda Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, kushiriki maandhimisho ya siku ya wanawake Duniani

Wito huo umetolewa na kaimu katibu tawala wa wilaya ya Dodoma mjini, Hemed Sebastian wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya uongozi kwa wanawake waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, mafunzo yaliyoandaliwa na jukwaa la wanasiasa wanawake (ULINGO) mjini hapa.

Amesema wanawake wana nafasi kubwa ya kudumisha amani kwa kufanya kampeni zao bila kuvunja amani na utulivu uliopo hapa nchini kwa kuwa kama kutatokea machafuko yoyote waathirika wakubwa watakuwa ni wanawake na watoto.

Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dk, Dinah mbaga amesema kuwa mafunzo hayo ni maalum kwa ajili ya wanawake na watu wenye ulemavu waliojitokeza kutangaza nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye vyama vyao kwenye ngazi ya ubunge na udiwani.