Wednesday , 8th Mar , 2017

Leo Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kote kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambapo Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameeleza jinsi serikali ilivyoweza kufanya makubwa kwa ajili ya wanawake.

Katika tamko lake kuhusiana na siku hii, Ummy amesema serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanashiriki na kunufaika na uchumi hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imejipanga kuelekea katika uchumi wa viwanda na kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Jukwaa la Uchumi Duniani kuhusu ‘Pengo la Jinsia ya Mwaka 2016’ inaonesha kuwa kutokana na jitihada zilizofanyika nchi yetu inashika nafasi ya 53 kati ya nchi 144 zinazofanya vizuri katika masuala ya jinsia Duniani.

Waziri Ummy Mwalimu

Haya ni baadhi ya mambo yaliyofanywa na serikali kwa ajili ya kuwainua wanawake kiuchumi.....

  • Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao unatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo kuanzisha na kuendeleza biashara, viwanda vidogo, kilimo pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi.

 

  • Halmashauri zimehamasishwa kuchangia asilimia tano ya mapato yao ya ndani ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016 kiasi cha shs. 4,102,808,513 kilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana katika Halmashauri 101 kupitia utaratibu huu.

 

  • Benki ya Wanawake Tanzania pia ilitoa mikopo yenye thamani ya Shs 9,323,240,000/-  kwa wajasiriamali 6,267 kati ya hao wanawake walikuwa 4,596. Hivyo, kiasi cha mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka Tshs. 112,473,600,000/- mwaka 2015 hadi kufikia Shs  121,796,840,000/-  mwaka 2016.

 

  • Idadi ya wajasiriamali waliopata na kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Wanawake Tanzania iliongezeka kutoka wajasiriamali 79,983 mwaka 2015 hadi kufikia wajasiriamali 86,250 mwaka 2016 ambapo asilimia 73 ya wanufaika wa mikopo hiyo ni wanawake.

 

  • Serikali imeratibu na kuzindua majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. Majukwaa haya yatatumika kama sehemu muhimu kwa wanawake wajasiriamali kukutana na kujadili fursa za kiuchumi pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.

  • Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002, (ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa za ajira kati ya wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, pale inapotokea mwanaume na mwanamke wanapata alama sawa wakati wa usaili, mwanamke anapewa kipaumbele kupata nafasi hiyo.

 

  • Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini (2004) imetoa fursa sawa kati ya wanawake na wanaume kuhusu haki zao za ajira, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.

 

  • Serikali inatekeleza sera ya Elimu bila malipo ambayo inatoa fursa ya Elimu ya Msingi na ya Sekondari na kuwahakikishia watoto elimu hiyo bila kujali tofauti za kiuchumi.

Katika ngazi za maamuzi na sheria mbalimbali, serikali imefanya yafuatayo....

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

  • Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1995 na ya mwaka 2005 yalifanywa na kuongeza idadi ya viti maalum kwa wanawake vilivyoongezwa hadi kufikia asilimia 30.

 

  • Katika kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao, sheria kadhaa zimetungwa na nyingine kufanyiwa marekebisho ikiwemo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana yaani (SOSPA) ya  mwaka 1998, ambayo imefanyiwa marekebisho  na kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu.

 

  • Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika ajira na likizo ya Uzazi pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009; Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, ambapo sheria hii inampa mwanamke haki ya kumiliki na kurithi ardhí sawa wanaume.

 

  • Pia, katika mwaka 2016/17 Bunge la Jamhuria ya Muungano limepitisha Sheria ya Msaada wa Sheria ya mwaka 2016 ambayo itasawadia wanawake hasa wenye kipato cha chini kupata haki zao za msingi.

 

  • Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22) ambao ulizinduliwa tarehe 13 Disemba, 2016.