Friday , 7th Oct , 2016

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kufungua Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya-NHIF hivi karibuni baada ya serikali hiyo kukaa muda mrefu bila ya kuwa na huduma za mfuko huo visiwani humo.

Mh. Mahmoud Thabit Kombo

Akizungumza hii leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya uwasilishwaji wa mada ya historia ya NHIF Tanzania bara na namna ya kufungua mfuko huo kwa upande wa Zanzibar iliyotelewa na kaimu mkurugenzi wa NHIF, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo amesema wazanzibari wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu hivyo kufunguliwa kwa bima ya afya kutawawezesha kujipatia huduma za matibabu yenye gharama nafuu.

Akifunga mjadala na uwasilishwaji wa mada uliohudhuriwa na waziri wa afya wa Zanzibar pamoja na kamati yake Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Mheshimiwa Anna Makinda ameeleza kuwa NHIF ipombioni kuweka utaratibu wa kuwawezesha wanachama wake kutibiwa matibabu popote walipo nchini tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo mwanachama anatibiwa ndani ya eneo lake la makazi.

“Ni lazima mambo mengine yabadilike kulingana na wakati, utaratibu wa kutibiwa eneo moja utaondolewa ili mwanachama hata akihama aweze kupata sifa ya kupokea matibabu popote alipo nchini” amesema

Aidha, Mheshimiwa Makinda ametoa wito kwa wakazi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kujiunga na mfuko huo wa NHIF pindi itakapo funguliwa ili waweze kuokoa maisha yao wakati wowote watakapohitaji msaada wa kimatibabu.