Monday , 30th Jul , 2018

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limesema lengo la kuwepo kwa utaratibu wa wasanii kuenda kuchukua kibali BASATA kabla hawajasafiri nje ya nchi ni kutaka kufahamu wanachokwenda kukifanya huko kwa madai wengine wanatumiwa kubeba dawa za kulevya katika safari zao.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Hayo yameelezwa na Afisa habari wa BASATA leo Julai 30, 2018, Bi. Agness Kimwaga wakati akizungumza na www.eatv.tv na kusema utaratibu huo sio mpya kufanyika ila umefanyiwa maboresho kidogo ambayo yanamtaka kila msanii kulipia fomu maalumu ya kibali hicho.

"Huu utaratibu siyo mpya kama baadhi ya wasanii wanavyosema huko kwenye mitandao, utaratibu huu upo siku zote. Msanii anapotaka kuenda kufanya show nje ya nchi anapaswa aje BASATA kujaza fomu maalum ambayo anakuwa anailipia shilingi elfu 50 ili kusudi aweze kupita 'airport' bila ya kuzuiliwa na watu wanaoshughulikia masuala haya..

lengo la kuwepo na utaratibu huu ni kutaka kufahamu anachokwenda kukifanya msanii huyo nje ya nchi maana wengine wamekuwa wakitumia safari hizo vibaya kwa kubebeshwa dawa za kulevya", amesema Bi. Agness.

Aidha, Bi. Agness amesema kupitia njia ya kibali wao kama BASATA wanao uwezo wa kumsaidia msanii endapo atapata shida huko alipo nje ya nchi kwa kuwasaliana na Balozi ya nchi iliyopo ili aweze kufika Tanzania kwa usalama lakini ikitokea ameenda kinyemela wao hawataweza kuhusika kwa lolote lile.

"Msanii akitudanganya kwamba anaenda nje ya nchi kwaajili ya mapumziko halafu tukapata taarifa kuwa amefanya 'show', sisi tutamsubiri arudi ndio tutamalizana naye. Pia hata kama atafanya vitu ambavyo ni kinyume na maadili yetu akirudi tu tutamshughulikia kama tulivyomfanyia Shilole kipindi kile", amesisitiza Agness. 

Kauli hiyo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limekuja baada ya kupita siku kadhaa tokea kuenea uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa miongoni mwa wasanii wakubwa wa bongo fleva nchini amezuiliwa uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam kutokana na kutokuwa na kibali kinachomruhusu kuenda kufanya show nje ya nchi.