
Ukilinganisha na mikoa mingine, Kigoma ilikuwa na mpangilio wa aina yake wa nyimbo ambapo kila msanii alijitahidi kupanga nyimbo ambazo mashabiki wanazijua ili kuamsha shangwe na wakati mwingine kuimba nao pamoja.
Ukiachana na Mzee Yusuph ambaye alifungua tamasha hilo, wasanii wengine kama Ben Pol, Amini, Mwasiti na Christian Bella, kuna wakati walilazimika kurudia nyimbo fulani mara mbili ili kuendelea kukonga nyoyo za mashabiki waliofurika katika Uwanja wa Lake Tanganyika kushuhudia onesho hilo ambalo hupita mikoani mara moja kwa mwaka na nyinginezo.
Wakati Christian Bella akikonga nyoyo za mashabiki kwa kibao cha Nani kama Mama, Mwasiti alishangiliwa katika kila wimbo aliokuwa makiimba kuanzia Hao, Mapito mpaka serebuka.
Naye Amini ambaye ni mara ya kwanza kupanda jukwaa la muziki la KiliKili Music Tour kwa mwaka huu alifanikiwa kuamsha mashabiki waliokuwa na kiu ya kumuona kwa nyimbo zake, Robo saa, Daima Milele.
Wasanii wengine ambao ilibidi wachague nyimbo chache kutokana na wingi wa nyimbo walizonazo, ni Profesa Jay, MwanaFA, Diamond na Weusi ambao walikuwa wakati mwingine wanaimba wimbo nusu na kuukata ili kukimbizana na muda, kwani onesho huwa linaenda masaa sita tu.
Onesho la mkoa wa Kigoma lilianza saa mbili kamili za usiku na kumalizika saa nane huku msanii wa mwisho kupanda jukwaani akiwa ni Naseeb Abdul ambaye alifanikiwa kukonga nyoyo na kumaliza tamasha kwa amani na kuwaacha mashabiki wakiwa wameridhika baada ya kuwa anafuata walichokuwa wakikimuelekeza.
Ziara hii imeacha gumzo kubwa Kigoma kwani mashabiki wengi walikuwa wanasbiri kwa hamu na wasanii wao hawakuwaangusha.
Ziara hii inaratibiwa na makampuni ya East Africa Tv na Radio, Executive Solutions, Aim Group, Integrated Communications na Aggrey and Clifford.
Baada ya Kigoma, Kili Music Tour sasa inaelekea Tanga Jumamosi ijayo ambapo burudani ya aina yake inatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Mkwakwani na baada ya hapo show kubwa ambayo ndio funga kazi na tayari ishaanza kuwa gumzo kubwa, itafanyika Dar es Salaam Septemba 6.
