Tuesday , 18th Jul , 2017

Mkongwe wa hip hop Bongo, Jay Moe amedai kuwa muziki kwa sasa umekuwa mgumu zaidi ukilinganisha na zamani hali ambayo imekuwa sababu kubwa  kuwaondoa baadhi ya wasanii wa zamani ambao wana uwezo mkubwa.

Jay Moe amesema kwamba mazingira ya kujitengeneza (brand) pamoja na kusukuma muziki ufike mbali ni changamoto kwa wasanii wakongwe kwani hawakuzoea masuala ya mitandao au video zaidi ya kuandaa ngoma kali zenye ladha ya kipekee.

"Muziki umekuwa mgumu kuliko zamani, ugumu wake ni kwamba zamani ulikuwa hauhitaji kufanya photo shoot, hauhitaji kuji-brand kwenye mitandao ya kijamii kudeal na video ukitoa tu ngoma kama 'Jua au Mvua', tulitengeneza CD tukasambaza kwenye redio tofauti na tuka-'hit' na tukaweza kuishi,” Jay Moe.

Pamoja na madai hayo Jay Moe ameongeza kwamba "Ukizungumzia muziki wa sasa hivi unaona wasanii wakali lakini wanashindwa kuingia ndani yake sababu ya mazingira ya game yalivyo. Game inahitaji vitu vingi ambavyo kuvifanya mpaka uwe na pesa, au uwe chini ya uongozi unaoweza kukugharamia,” amesisitiza