Monday , 14th Aug , 2017

Rais wa Manzese, Madee anayetamba na ngoma mpya 'Sikila' amedai hajawahi kumuomba ushauri mtu  ili apate ujasiri wa kuachia ngoma yake mpya ambayo imekaa tofauti kwenye video  kwani yeye tayari ana serikali yake anayoiamini kabla ya kuomba ushauri.

Madee ametoa kauli hiyo leo wakati akijibu swali la mtangazaji wa kipindi cha Planet Bongo ya East Africa Radio, Abdallah Ambua wakati alipohoji ni wapi alipotoa ujasiri wa kuachia video yenye mahadhi ya katuni tofauti na zilizozoeleka.

"Huwa najiamini kabla ya kumuamini mtu mwingine yeyote. Huwa siombi ushauri kwa watu kabla serikali yangu kichwani haijaamua. Maamuzi yangu nayaamini sana hivyo mawazo ya watu wengine huwaga ya ziada sana lakini mimi napenda kufanya vitu vya tofauti ndiyo maana hata hii video ni ya tofauti lakini nimethubutu" Madee.

Aidha katika wimbo wake mpya aliyomshirikisha mwanamuziki Tekno toka Nigeria Madee amesema amefunguka siri ya yeye kuendelea kuwepo kwenye game muda mrefu ni kutokana na yeye kupenda kufanya vitu ambavyo watu wanaviogopa.

Madee amefunguka na kusema kwamba anafahamu ana mashabiki wengi ambao  wengi wao wanampenda sana akiwa ana-rap lakini kutokana na uwepo wake kwenye sanaa muda mrefu anafahamu pia wapo ambao hawapendi kumsikia katika muziki huo.

"Napenda kufanya kitu ambacho sijawahi kufanya katika maisha yangu ya muziki. Utofauti wangu ndiyo unaonifanya hata sasa niwepo kwenye game nipambane na vijana waliopo. Najua wapo watu wengi ambao wanampenda Madee anaye-rap na nikiimba nawapoteza lakini na upande wa pili ni hivyo hivyo ndiyo maana nabadilika mara kwa mara." alisisitiza Madee.