Sunday , 2nd Dec , 2018

Klabu ya soka ya Mbeya City imeibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 katika mchezo wake wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya African Lyon hii leo.

Wachezaji wa Mbeya City

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, umeshuhudia vijana hao wa kizazi kipya wakipata ushindi wa kwanza mkubwa msimu huu, mabao yaliyofungwa na Idd Nado katika dakika ya 2 na 20, Hangaya katika dakika ya 23 na Eliud Ambokile aliyefunga katika dakika ya 28. Bao pekee la African Lyon likifungwa na Adam Omary katika dakika ya 90.

Mshambuliaji wa klabu hiyo, Eliud Ambokile sasa amefikisha jumla ya mabao 9 ya ligi kuu Tanzania bara na kuwaacha washambuliaji hatari wa vilabu vikubwa vya Simba, Yanga na Azam FC. 

Wanaomfuatia kwa karibu katika listi ya wafungaji bora wa TPL ni pamoja na Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wa Simba, Said Dilunga wa Ruvu Shooting na Heritier Makambo wa Yanga wote wakiwa na idadi ya mabao 7. 

Baada ya ushindi huo wa Mbeya City sasa inafikisha alama 22 katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi. 

Matokeo mengine ya michezo ya leo ni pamoja na JKT Tanzania ambayo imetoka sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting, Kagera Sugar imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Alliance FC, Ndanda FC imetoka suluhu na Mbao FC pamoja na mchezo wa Lipuli FC dhidi ya Biashara United ambao umeahirishwa katika dakika ya 28 kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mjini Iringa. Mchezo huo utarudiwa kesho Disemba 3 katika uwanja wa Samora.