Tuesday , 23rd Aug , 2016

Timu ya Yanga ya Dar es Salaam imeaga mashindano ya kombe la shirikisho kwa kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa TP Mazembe ya DRC.

Mechi hiyo ya marudiano ya Kundi A ambayo imepigwa mchana wa leo Lubumbashi nchini DRC, ilikuwa na umuhimu wa kuweka heshima kwa Yanga kwa kumaliza ikiwa na point 7 jambo ambalo limeshindikana.

Katika mchezo huo uliokuwa na kasi ya aina yake huku Yanga ikionesha uhai katikamuda wote wa mchezo, ilijikuta ikianza kubugia mvua ya mabao kuanzia dakika ya 28 kwa bao lililofungwa na Bolingi.

Wakati Yanga ikijipanga kutafuta bao la kusawazisha katika kipindi cha pili, Reinford Kalaba akapiga bao la pili katika dakika ya 55, na baadaye dakika ya 64, huyohuyo Kalaba akaipatia Mazmbe bao la 3.

Dakika ya 68 Yanga ilifanya mabadiliko ya kumtoa Simon Msuva na kumuigiza Juma Mahadhi, mabadiliko ambayo yalizaa matunda matunda.

Yanga ilipata bao lake la kufutia machozi katika dakika ya 75 kupitia kwa Amis Tambwe baada ya kuunganisha vyema mpira wa adhabu uliopigwa kiufundi na na Haruma Niyonzima.

Katika mchezo mwingine, Medeama ya Ghana imekubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa MO Bejaia nchini Algeria, na kufanya msimo wa kundi A ubadilike, hali iliyopelekea Medeama kuungana na Yanga kufungasha virago.

Msimamo wa kundi hilo unaonesha kuwa TP Mazembe ndiyo vinara wakiwa na point 13 wakifuatiwa na MO Bejaia yenye point 8 ikilingana na Medema yenye point 8 pia, huku wakilingana tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, na Yanga inakamata mkia ikiwa na point 4.

MO Bejaia imefuzu kutokana na matokeo kati yake na Medeama ambapo katika mechi mbili ambazo wamekutana, MO Bejaia imevuna point 4 huku Medeama ikiambualia point 1.

TP Mazembe na MO Bejaia zinafuzu nusu fainali ya michuano hiyo.