
Adriano anakuwa mchezaji wa 3 wa Barcelona kukumbwa na kesi za ukwepaji kodi katika kipindi hiki ikiwa ni wiki chache tu kabla star wa klabu hiyo Lionel Messi kuanza kusikilizwa kwa kesi yake ya mashitaka kama hayo.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka, Adriano ambaye ni raia Brazil, alikwepa kulipa kodi ya Euro 646,086 kati ya mwaka 2011 na 2012 aliposhindwa kubainisha mapato yake kutokana na haki miliki zake za picha na matangazo yake.
Licha ya Adriano kulipa deni hilo baada ya kufunguliwa mashitaka, mchezaji huyo ataendelea na kesi yake na kuna uwezekano kuwa atapigwa faini.
Mkasa huu umekuja wakati Messi na baba yake mzazi, Jorge, wakijitayarisha kwenda mahakamani wakidaiwa kukwepa kulipa kodi ya Euro Milioni 4.16 kwenye kipindi cha 2007 na 2009 iliyotokana na haki miliki za picha na matangazo ya Messi.
Messi alikana mashitaka yote akijitetea kuwa baba yake ndiye anayesimamia masuala yake yote ya mapato yake.