Sunday , 17th Sep , 2017

Hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika mkondo wa kwanza imeendelea usiku wa kuamkia leo kwa timu ya Al Ahly kulazimishwa sare kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Mabingwa hao wa soka wa Misri waliikaribisha ES Tunis ya Tunisia kwenye dimba la Borg El Arab. Al Ahly walipata bao la kuongoza dakika ya 10 kupitia kwa Abdallah El-Said kwa penalti kabla ya Yassine Khenissi kuisawazishia ES Tunis dakika 10 baadae.

Dakika ya 48 kipindi cha pili, Ghilane Chaalali aliiandikia ES Tunis bao la pili kufuatia makosa ya golikipa wa Al Ahly, Sherif Ekramy ambaye alidaka mpira wa adhabu ndogo na kisha kuuachia kwa makosa ukaingia nyavuni na kufanya ES Tunis waongoze 2-1.

Walid Azaro aliisawazishia timu yake ya Al Ahly dakika za mwisho hivyo kufanya mchezo wa marejeano mjini Tunis kuwa mgumu. Katika robo fainali nyingine USM Alger ya Algeria imeilazimisha sare ya 1-1 Ferroviario Beira ya Msumbiji.

Mechi za leo Robo Fainali ni Mamelodi Sundowns vs WAC Casablanca pamoja Al Ahly Tripoli vs Étoile du Sahel.