Wednesday , 31st May , 2017

Kipa mkongwe wa Yanga, Ally Mustapha 'Barthez' na beki wa pembeni wa timu hiyo, Oscar Joshua ni kati ya wachezaji watakaokuwepo kwenye kikosi cha Singida United katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, vinginevyo safari yao na Yanga itakuwa imekwisha.

Kipa namba mbili wa Yanga Ally Mustafa 'Bartez'

Barthez na Joshua ni kati ya wachezaji ambao hawakuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Mzambia, George Lwandamina katika msimu uliopita wa ligi kuu na mpaka sasa bado wana mikataba ya mwaka mmoja wa kuichezea Yanga.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani wachezaji hao wataondolewa Yanga na kupelekwa Singida United inayofundishwa na Kocha Mkuu Mholanzi, Hans Pluijm aliyekuwa anaifundisha timu hiyo kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na George Lwandamina.

Mtoa taarifa huyo amesema, wachezaji hao walikuwepo kwenye orodha ya wachezaji watakaochwa katika msimu ujao, lakini kutokana na mikataba yao kutomalizika watapelekwa kwa mkopo.

"Barthez na Joshua hawana nafasi ya kucheza katika kikosi cha Lwandamina na pia hana mipango nao, hivyo kama uongozi tumeona ni vyema ukawatoa kwa mkopo. Tutawatoa baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Singida na kukubali kuwachukua, hivyo tumeona tuwaachie waende huko wakacheze," amesema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Barthez kuzungumzia hilo amesema "Bado sijapata taarifa rasmi ya kupelekwa kwa mkopo, ni tetesi ninazozisikia pekee kama ulivyosikia wewe ni vema tukasubiria kwanza kabla ya mimi kuongea chochote. Kingine ni ngumu mimi kuondoka kabla ya kupelekwa huko na Yanga, kama unavyojua bado nina mkataba wa kuichezea Yanga,"