
Makamu wa Rais wa ZFA Haji Amery Haji amesema tamko la Malinzi la kusema ataipeleka ZFA Shirikisho la soka Barani Afrika CAF,ili Zanzibar ifutwe uanachama kama haitofanya uchaguzi wa ZFA,ni kauli ya uchochezi na hawaiogopi.
Haji ambaye alibaki ndani ya ZFA kusimamia mchakato wa kuundwa kamati ya muda,kuandaa katiba na tarehe ya uchaguzi,amesema Malinzi amekuwa msaliti kwa kuwa hata yeye alishiriki vikao vya kuleta suluhisho la mzozo huo,na akaagiza yafanyiwe kazi mapendekezo ya kuandaa uchaguzi,lakini leo anesema haitambui kamati hiyo.
Haji pia ameibua swala lingine la utumiaji mbaya wa fedha za FIFA kwa Jamal Malinzi,ambapo alimpa dola 2000 Rais wa ZFA Ravia Hidarous aitishe mkutanao Mkuu wa ZFA,fedha ambazo hazikupitia benki.
Haji amesema fedha hizo zinachunguzwa na taarifa imeshafika Polisi,huku TFF ikiwa haionyeshi ushirikiano wowote.
Haji amesema Malinzi amejitumbukiza kumuegemea Rais wa ZFA,ambaye ana kesi ya kuingiza siasa kwenye soka,ambapo rais huyo wa ZFA alidiriki kusema Zanzibar haitocheza mpira hadi Muungano uvunjike au kuwe na serikali tatu.
Haji akamalizia kwa kusema kuwa Malinzi anatakiwa kuomba radhi na asipofanya hivyo watampeleka Mahakamani kwa kuwaunga mkono watu wanaochochea kuvunjwa kwa Muungano.