Sunday , 30th Dec , 2018

Kocha wa klabu ya Simba, Patrick Aussems amesema kuwa anaamini klabu yake inaweza kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Kocha Patrick Aussems

Kauli hiyo ameizungumza katika mkutano na wanahabari baada ya ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United, uliopigwa jana Jumamosi.

Aussems amesema kundi la Simba katika Klabu Bingwa liko wazi na yeyote anaweza kupata nafasi ya kufuzu lakini akiamini timu yake inayo nafasi kubwa kutokana na sapoti kubwa ya mashabiki hasa katika michezo ya nyumbani.

"Nafikiri ni kundi ambalo liko wazi, hata kama tuko na timu mbili ambazo zilicheza fainali msimu uliopita. Timu hizi zimecheza mechi ngumu sana katika siku za karibuni na hazitakuwa na muda wa kupoteza," amesema Aussems.

"Na hii ni droo nzuri kwetu, mimi nina uhakika endapo tutacheza mbele ya mashabiki zaidi ya elfu 60 kama tulivyofanya dhidi ya Nkana Red Devils, nina uhakika mkubwa kuwa tutafika robo fainali hata kama timu hizi zina uzoefu mkubwa kuliko sisi lakini sisi pia tuna wachezaji wazuri," ameongeza.

Simba imepangwa kundi D pamoja na Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Congo DRC na JS Saoura ya Algeria.

Al Ahly ilicheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Esperance Tunis ya Tunisia ambapo Esperance ilishinda ubingwa kwa uwiano wa mabao 4-3 huku AS Vita Club ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.