Tuesday , 13th Nov , 2018

Uongozi wa kampuni ya Football House, inayommiliki mchezaji chipukizi wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' umesema unafanya kila jitihada kuhakikisha mchezaji huyo anapata timu itakayotimiza malengo yake.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya vijana U17 (Serengeti Boys), Kevin John

Kevin John amerejea nchini wiki hii akitokea nchini Denmark katika klabu ya HB Koge ambako alikwenda kufanya majaribio kwaajili ya kujiunga na klabu hiyo. Taarifa zinaeleza kuwa mchezaji huyo amefuzu majaribio na kinachosubiriwa kwa sasa ni mazungumzo baina ya klabu hiyo na kampuni inayommiliki.

Akizungumza juu ya maendeleo ya mchezaji huyo kwa sasa baada ya kurejea nchini, Mkurugenzi wa Football House, Mbaki Mutahaba amesema,

"Sisi tulichokuwa tunataka sanasan ni mtoto aende kule mapema zaidi, kwenye nchi ambayo inaweza kumuendeleza vizuri zaidi, kwahiyo yule anayeweza kumuendeleza kwa mazingira ambayo ni bora zaidi, huyo ndiye asilimia kubwa tutakayeenda naye," amesema Mutahaba.

Naye mwakilishi aliyekwenda na mchezaji huyo katika majaribio yake nchini Denmark, Jamal Baras amesema kuwa majaribio ya Kevin John yameonesha matumaini makubwa japokuwa klabu haijatoa ripoti rasmi.

"Nilikuwa napata maoni japokuwa hayakuwa rasmi, lakini yameonesha amefanya vizuri na nashukuru Mungu baada ya kumaliza tuliweza kupata 'Full Evaluation' tathmini kamili pamoja na barua rasmi iliyokwenda kwa Football House inayoonesha kuwa wameridhika naye na wangependa aweze kucheza," ameongeza.