Thursday , 31st Jan , 2019

Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Aussems ameelezea kuhusiana na programu ya mazoezi ya siku ya kwanza baada ya kuwasili nchini Misri kwaajili ya mchezo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.

Kocha, Patrick Aussems na wachezaji wakiwa mazoezini

Akizungumza kupitia mitandao ya kijamii ya Simba, baada ya mazoezi ya usiku, Aussems amesema kuwa baridi ndilo jambo lililowapa changamoto lakini kwa siku watakazokuwepo, watazoea na kuwa fiti kwa mchezo huo.

"Usiku wa leo ( jana ) tumekuwa na programu nzuri ya mazoezi, tumekuwa na kipindi cha kutazama video mbalimbali pia ili kuwaonesha vijana nini wanatakiwa kufanya. Japo kuna changamoto ya baridi, wanahitaji joto lakini tumekwenda vizuri", amesema.

Akizungumzia urejeo wa mshambuliaji, John Bocco, kocha Aussems amesema kuwa anafurahi kuona urejeo wa mchezaji huyo na atamtumia kama moja ya silaha kubwa kuelekea mchezo huo.

"John amerejea kujiunga na sisi, kwahiyo ni moja ya silaha ambayo tunaihitaji. Ni mchezaji mzuri kwenye timu yetu na atatusaidia kwenye michezo", ameongeza.

Simba inatarajia kupambana na wenyeji Al Ahly katika mchezo wa Klabu Bingwa Barani Afrika Februari 2, mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Borg El Arab.