Wakufunzi wa soka la Vijana kutoka Klabu ya Manchester United wakiwa katika uwanja wa Azam Complex Chamazi DSM
Ile kliniki maalum ya mafunzo kwa vijana wa Aitel Rising Stars inayoendeshwa na makocha kutoka klabu ya Manchester United…imefanyika leo katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Akiongea na EATV, mgeni rasmi katika kliniki hiyo, naibu waziri wa mambo ya nje mh. Mahadhi J. Maalim amepongeza juhudi za waandaaji wa kliniki hiyo na watu wote waliohusika katika kufanikisha na kuongeza kwamba maendeleo ya michezo hapa nchini yanategemea juhudi za wadau wote na wala sio kuisubiri serikali ifanye kila kitu.
Kliniki hiyo inashirikisha vijana 72 wa kike na kiume kutoka mataifa 12 barani Afrika ambapo katibu mkuu wa shirikisho la soka hapa nchini TFF bwana Celestine Mwesiga ameleezea faida za vijana wa kitanzania kuchanganyika na vijana wa mataifa mengine kwamba itawafanya wajue jinsi wenzao wa mataifa mengine wanavyocheza mpira hivyo kuwafumbua kimchezo.
Naye mwenyekiti wa kamati ya soka la vijana ya shirikisho la soka hapa nchini TFF bwana Ayoub Nyenzi ameelezea faida ya jumla kwa kliniki hiyo kufanyika hapa nchini kwamba imetoa fursa kwa vijana wengi wa kitanzania tofauti na mataifa mengine, Tanzania imetoa watoto 19 kati yao wavulana 3 na wasichana 16. Zaidi ya hapo makocha watatu wa kitanzania watapatiwa mafunzo maalumu ya kuboresha uwezo wao wa kuwafundisha vijana.
Aidha makocha kutoka Manchester United wakiongozwa na Neil Scott wameelezea faida za kliniki hiyo kwa vijana waliohudhuria kwa kusema wao wanawafundisha vijana hao falsafa ya uchezaji wa Manchester United hivyo itawasaidia kuongeza juhudi wakiwa na ndoto za kuichezea timu hiyo siku moja