Saturday , 1st Jul , 2017

Timu ya The Fighter imekuwa ya kwanza kuyaaga mashindano ya Sprite BBall Kings baada ya kuchapwa kwa pointi 109-41 dhidi ya Mchenga BBall Stars katika hatua ya robo fainali mchezo uliopigwa katika viwanja vya Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) leo.

 Nahodha wa timu ya iliyopenya ambayo ni  Mchenga BBall Stars, Mohamed Yusufu amesema licha ya mchezo kuwa mgumu kwa kipindi chote lakini waliweza kuwasoma wapinzani wao vizuri jambo ambalo liliwasaidia kupata ushindi huo.

"Tumeweza kutumia madhaifu ya wapinzani wetu waliyokuwa wanaonesha uwanjani kama njia ya kujipatia ushindi huu ila tunamshukuru Mungu kwa kuweza kufuzu hatua hii na kuingia nusu fainali ya michuano hii", alisema Mohamed.

Kutokana na ushindi huo Mchenga BBall Stars imeweza kujikatia tiketi ya moja kwa moja kuingia kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hii inayoendelea kurindima mchana huu kati ya Flying Dribblers dhidi ya Osterbay.

Pamoja na hayo, Mchenga team wameweza kutoa mfungaji bora Rwahabura Munyagi kwa siku ya leo 'best scorer' kwa pointi 25 huku  mpinzani wake Martin Kolikoli akipata pointi 12 kutoka The Fighter

Mtanange huo uliojaa upinzani mkubwa kwa kila mmoja kutaka kupata ushindi umechezeshwa na refa Shaban Mohamed pamoja na msaidizi wake 'Empire' Edwin Kilagwa.