Saturday , 1st Jul , 2017

Michuano ya mpira wa kikapu ya 'Sprite BBall kings' iliyochezwa leo katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hatimaye imemalizika huku timu nne pekee kati ya nane zikiwa zimefuzu kuingia hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Miongoni mwa Nahodha wa timu zilizoweza kutinga nusu fainali Geofrey Lea kutoka Flying Dribblers amesema haikuwa jambo rahisi kwa timu yake kupata ushindi mbele ya wapinzani wao Osterbay kwa kuwa nao walikuwa wanafanya mashambulizi ya hatari kila muda japokuwa wametoka katika kinyang'nyiro hiki.

"Tumeweza kufuzu katika mashindano haya kutokana na kupata fursa nzuri ya kufanya mazoezi kwa muda wote ambapo imeweza kuimarisha kiwango chetu kwa hali juu tofauti na tulivyokuwa katika mechi zilizopita tulionekana kutofanya vizuri wakati wote uwanjani kwa sababu ya kuwa wageni katika mashindano haya", alisema Lea. 

Hata hivyo kwa upande wa timu zilizotolewa kwenye michuano hii wamesema sababu kubwa ya wao kufungwa ni kutokana na makosa madogo madogo ya kiufundi pamoja na uchezaji mbaya wa wachezaji wao jambo ambalo lililopelekea kupigwa adhabu nyingi mara kwa mara na kusababisha wachezaji bora kupewa kadi nyekundu na kupoteza mchezo mzima.

Mchezaji wa Kigamboni Heroes akiwa ameweka kizingiti asipite mchezaji wa Kurasini Heat

Kwa upande mwingine, haya ndiyo matokeo ya timu zote zilizoweza kucheza siku ya leo ambapo Mchenga BBall Stars waliifunga  The Fighter kwa'point' 109-41, TMT walipata 96- 73 dhidi ya Dream Cheaser huku Flying Dribblers wakiwafunga Osterbay kwa point 91- 81 na kumaliziwa mtanange huo kwa  Kurasini Heat kumchakaza Kigamboni Heroes kwa pointi 64-59.