Wednesday , 3rd Jan , 2018

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola ameweka wazi kuwa mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Brazil Gabriel Jesus atakuwa nje kwa wiki sita na huenda akarejea kwenye mechi za UEFA.

Guardiola ametolea ufafanuzi majeraha ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye aliteguka goti kwenye mchezo dhidi ya Crystal Palace Disemba 30 mwaka jana.

"Baada ya vipimo ripoti ya daktari imeonesha ameteguka goti lakini matibabu yake hayahitaji upasuaji na atakuwa nje kati ya wiki nne hadi sita'' amesema Guardiola kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya ushindi wa 3-1 iliopata timu yake dhidi ya Watford usiku wa kuamkia leo.

Kocha huyo raia wa Hispania ameongeza kuwa anatarajia kuwa na nyota huyo mapema mwezi Februari kabla ya mechi ya ligi ya mabingwa hatua ya 16 dhidi ya FC Basel Februari 16. 

Baada ya ushindi wa jana Man City sasa imefikisha mechi 22 bila kupoteza huku ikiendelea kujikita kileleni kwa kufikisha alama 62, ikiwa ni alama 15 juu ya Manchester United inayoshika nafasi ya pili na alama 47.