
Kikosi cha Mtibwa Sugar
Hatua hiyo imekuja baada ya kupewa taarifa kuwa uwanja wake wa Jamhuri Morogoro haukidhi vigezo vya kuchezea michezo ya kimataifa.
Akizungumza mjini Morogoro, Mkurugenzi wa klabu hiyo, Jamal Bayser amesema kuwa awali walipanga kutumia uwanja wa Jamhuri Morogoro kwaajili ya michezo hiyo lakini kutokana na mahitaji ya TFF na CAF imewalazimu kuhamishia katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es salaam.
"Bahati mbaya tumeambiwa na TFF kuwa uwanja wetu haukidhi vigezo vya CAF kwahiyo hauruhusiwi kwa michezo ya kimataifa, tumelazimika tuje tuchezee Dar es salaam na tulitaka tuchezee katika uwanja wa taifa lakini napo tumeona uwanja wa taifa umekuwa na gharama nyingi sana, kwahiyo tumeamua mechi zetu tucheze katika uwanja wa Chamazi Complex" amesema.
Mara ya mwisho kwa Mtibwa Sugar kushiriki michuano ya kimataifa ni mwaka 2003, ambapo katika mwaka huohuo ilifungiwa na CAF kutokana na kushindwa kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya klabu ya Santos ya Afrika Kusini.
Imepata nafasi ya kushiriki michuano ya shirikisho barani Afrika msimu huu baada ya kushinda ubingwa wa 'Azam Federation Cup' AFC msimu uliopita kwa kuichapa Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali, ambapo katika hatua ya awali ya michuano hiyo itavaana na Northern Dynamo ya Seychelles.