Tuesday , 6th Sep , 2016

Serikali imesema imedhamiria kuwekeza katika sekta ya michezo kwa maendeleo ya taifa kwa kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo Miundombinu ya michezo, elimu ya michezo, na kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha sekta ya michezo inaendelezwa/

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye.

Akitoa ufafanuzi leo bungeni kwanini sekta ya michezo inasuasua nchini Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye amesema mwaka huu serikali ilisimamisha michezo ya UMITASHUMTA NA UMISETA, ili serikali iweze kujipanga kutoa matunda bora zaidi kupitia mashindano hayo.

Waziri Nnauye amesema kuwa kwa muda mrefu mashindano hayo yamekuwa hayatoi maendeleo chanya kwa nchi lakini serikali imepania kuwaendeleza zaidi wanamichezo watakao patikana kupitia mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kuwaandilia shule maalum kwa kuendeleza vipaji vyao.

Aidha Mhe. Nape ameongeza kuwa, serikali kupitia bajeti yake ya wizara itaendeleza sekta ya michezo huku akiwataka wadau wote wa michezo ikiwemo taasisi za kiserikali kuibua vipaji na kuviendeleza ili kukuza na kuboresha sekta hiyo.

Mhe. Nape ameongeza kuwa serikali itatafuta vyanzo vingine vya mapato ikiwemo sekta binafsi pamoja na michezo ya bahati nasibu nchini kama wanavyofanya nchi nyingine ili kuboresha zaidi tasnia ya michezo nchini.