Wednesday , 2nd Nov , 2016

Vita kubwa kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara imeendelea kurindima kwenye viwanja sita hii leo huku vinara wa ligi hiyo Simba SC wakiendelea kuwaacha kwa mbali wapinzani wao Yanga.

Shiza Kichuya (Kulia) akishangilia bao

Simba imeichapa Stand United katika dimba la Kambarage Shinyanga bao 1-0 likifungwa na Shiza Kichuya dakika ya 31 kwa mkwaju wa penati baada ya Laudit Mavugo kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Wakati Simba ikikomba point 3 za mchezo wa leo, wenzao wana Jangwani wameangukia pua katika dimba la Sokoine Mbeya kwa kupigwa mabao 2-1 na Mbeya City, na kuifanya iwe nyumakwa point 8 kati yake na vinara Simba SC.

Hata hivyo mchezo huo ulikumbwa na rapsha za hapa na pale, hasa baada ya Mbeya City kupata bao la pili, ambalo Yanga waliligomea na kisha mwamuzi kulifuta, lakini baada ya wachezaji wa Mbeya City kulidai tena kwa mwamuzi bao hilo, alijadiliana na wasaidizi wake na kuamua kuwa lilikuwa goli halali.

Donald Ngoma - Yanga

 

Matajiri wa Chamazi, timu ya Azam pia imeendelea kujikusanyia point baada ya leo kuipiga Toto Africans katika dimba la CCM Kirumba Mwanza, na kuifanya iwe imekusanya point Sita kutoka Mwanza na Kagera kama ilivyokuwa kwa Yanga.

Michezo mingine iliyopigwa leo, Majimaji imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu mjini Songea, Ndanda FC pia ikiwa nyumbani imeichapa Tanzania Prisons bao 1-0 na Ruvu Shooting imekamatia point zake 3 kwa kuiadhibu African Lyon bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Mabatini mkoani Pwani.