Wednesday , 14th Nov , 2018

Klabu ya soka ya Singida United imeeleza mipango yake ya usajili wakati wa dirisha dogo ambapo imeweka wazi kuwa wameshaondoka wachezaji 11 hivyo wanajipanga kuziba nafasi zao kwa kusajili wachezaji wa kimataifa.

Mkurugenzi mtendaji wa Singida United Festo Sanga

Akiongea leo na www.eatv.tv mkurugenzi mtendaji wa Singida United Festo Sanga, amekiri kuwa kweli wachezaji wamekuwa wakiwadai pesa zao za usajili na wengine za mishahara lakini wamejifunza aina ya wachezaji na hawatawahitaji tena wachezaji ambao sio wavumilivu.

''Singida United itaimarika vizuri baada ya dirisha dogo kwani tunahitaji kuwaacha wachezaji 20 na tayari 11 ambao wamekosa uvumilivu wameshaondoka hivyo tutawaondoa wengine na tutasajili wachezaji wapya ambao wapo kwaajili ya kucheza na sio kuondoka'', amesema.

Aidha Sanga amesema katika dirisha dogo linalofunguliwa kesho Novemba 15 hadi Desemba 15, wamepanga kuboresha zaidi eneo la ushambuliaji ili kumpunguzia mzigo mchezaji Habibu Kiyombo.

Pia Sanga amesema wapo kwenye mazungumzo na wachezaji wanne wa kimataifa ambapo tayari wameshamalizana na mmoja kutoka Norway na muda si mrefu watamtangaza.