Sunday , 18th May , 2014

Taifa Stars imeanza vizuri hakati za kutafuta nafasi ya kufuzu kombe la mataifa Afrika nchini Morocco mwakani baada ya kuifunga Zimbabwe bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza iliyochezwa katika uwanja wa Taifa jijini DSM.

Baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars muda mfupi kabla ya kuanza kwa pambano dhidi ya Zimbabwe

Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imeanza vizuri hakati zake za kutafuta nafasi ya kufuzu kombe la mataifa Afrika baada ya kuifunga Zimbabwe bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza iliyochezwa katika uwanja wa Taifa jijini DSM.

Bao pekee la Taifa Stars limefungwa na John Bocco katika dakika ya 15 ya mchezo baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Mbwana samata na thomas ulimwengu.

Katika muda wote Taifa Stars ilionekana kucheza kwa uhai na tahadhari kubwa ambapo safu yake ya ushambuliaji ilikuwa ikiongozwa na Mbwana samata na Thomas Ulimwengu waliojiunga na timu jana wakitokea katika klabu ya TP Mazembe ya DRC.

Hata kipindi cha pili kilipoanza, Taifa Stars iliendelea kucheza kandanda la kuvutia na kuzidi kusukuma mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Zimbabwe na kukosa nafasi kadhaa za kufunga zikiwemo ya John Bocco na Mrisho ngassa.

Mchezaji Thomas Ulimwengu ndiye aliyeongoza kwa kuchezewa madhambi katika mchezo huo akiwa amedondosha takribani mara 9 na mabeki wa Zimbabwe.

Kikosi cha Stars kilichoanza katika mchezo wa leo, ni kama ifuatavyo: Godfrey Mnisi "Dida", Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub "Cannavaro", Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Mbwana Samata na Tomas Ulimwengu.

Mabadiliko yaliyofanyika katika mchezo huo ni pamoja na Hamis Mcha kuchukua nafasi ya John Bocco, Haruna Chanongo kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa na Amri Kiemba aliingia kuchukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto.

Baada ya mchezo huo walimu wote wawili walizungumza na waandishi wa habari ambapo kocha wa Taifa Stars Mart Nooij alisema kuwa alifahamu toka awali kuwa Zimbabwe watakuwa na timu ngumu kwa hivyo matokeo ya leo ni mazuri kwa Tanzania na atahakikisha timu inayalinda katika mchezo wa marudiano..

Alipoulizwa kuhusiana na sababu za kumtoa Mwinyi Kazimoto jambo ambalo halikuwafurahisha mashabiki wengi waliokuwa uwanjani, Nooij alijibu “Sikupi cha kuandika gazetini. Furahi nchi yako imeshinda”.

Kuhusu mbinu atakayotumia katika mchezo wa marudiano, Nooij amesema kuwa atahakikisha timu inacheza mpira na si kulinda lango.

Katika mchezo wa marudiano, Tanzania inahitaji sare ya aina yoyote ili kusonga mbele.

Endapo Tanzania itafanikiwa kuitoa Zimbambwe itakutana na mshindi kati ya Sudani Kusini na Msumbiji.

Mechi hiyo imechezeshwa na waamuzi kutoka Ghana wakiongozwa na Joseph Odartei Lamptey.