Wednesday , 25th May , 2016

Sherehe za tuzo za Wanamichezo Bora zinazotolewa kila mwaka na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA zitafanyika Agosti 26, mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika jana mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Juma Abbas Pinto.

Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo kwamba chama kimeandaa kamati maalum kwa ajili ya kusimamia upatikanaji wa wanamichezo hao bora.

TASWA hutoa tuzo kwa wanamichezo bora wa kila mchezo na pia kunakuwa na mwanamichezo bora wa jumla kwa mwaka husika.

Baadhi ya waliopata kutwaa tuzo ya Mwanamichezo Bora Tanzania wa jumla kwa miaka kumi iliyopita na miaka yao katika mabano ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007) na Mary Naali (2008) wote wanariadha.

Mwaka 2009 tuzo ilienda kwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan, ambaye pia alitwaa tuzo hiyo mwaka 2010, wakati mwaka 2011, ambapo tuzo yake ilitolewa mwaka 2012 mshindi alikuwa mwanasoka Shomari Kapombe na mwaka 2013/2014 ilienda kwa mwanasoka Sheridah Boniface.

Mwaka 2015 tuzo ilifanyika katika aina nyingine, ambapo walizawadiwa wanamichezo 10 tu waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 ya urais wa Jakaya Kikwete na pia TASWA ilitoa Tuzo ya Heshima kwa Kikwete.