Wednesday , 25th Mar , 2015

Klabu ya Yanga imepinga mabadiliko ya 37 kifungu cha tatu cha kanuni ya kuomba mchezaji mwenye kadi tatu za njano kuchagua mechi za kucheza yaliyofanywa na Bodi ya Ligi nchini na Shirikisho la Soka nchini TFF.

Akizungumza jijini Dar es salaam, kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Sheria wa Klabu Yanga, Frank Chacha, Mkuu wa Kitengo cha habari cha Klabu hiyo, Jerry Murro amesema, kifungu hicho kilirekebishwa Februari 08 mwaka huu na wao walipata taarifa Machi 14 mwaka huu huku kanuni hiyo ikiwa imeshaanza kutumika kwa muda wa mwezi mmoja tangu kufanyika kwa marekebisho hayo.

Murro amesema, klabu hiyo inapinga mchakato na matumizi ya kanuni hiyo kwani mchakato mzima uliopelekea mabadiliko haya na timu nyingine kuanza kuutumia bila taarifa kamili kutolewa kwa vilabu vyote haukuwa halali wala na hoja ya msingi.

Murro amesema, mchakato huo haukuhusisha wala kuangalia mahitaji ya wadau ambao ni timu zote shiriki za Ligi kuu Soka Tanzania bara kwa sababu mabadiliko haya hayakutokana na mahitaji wala kuombwa na vilabu hivyo hakukuwa na ulazima kubadilisha na mabadiliko hufanyika pale mahitaji yanapotokea.

Murro amesema, TFF lazima izuie kanuni hii na mchakato uanze upya ikiwa ni pamoja na kuifutia Pointi timu iliyotumia kanuni hiyo kwani kanuni hii imekuja katikati ya ligi na wachezaji wengine walipumzishwa kutokana na kuwa na kadi.

Murro amesema, kamati ya utendaji haikuzingatia sheria za kufanya mabadiliko ya kanuni kwani mabadiliko ya kanuni yanatakiwa yafananishwe na matumizi ya kanuni husika katika nchi nyingine.

Murro amesema, kamati iliyosimamia mchakato wa kubadili kanuni hiyo, imekiuka baadhi ya taratibu na kanuni muhimu za maadili za Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA na TFF katika kuongoza mpira wa miguu kwa kuvunja kanuni za maadili ambazo ni hadhi na maadili, haki sawa kwa wote katika soka ambapo mabadiliko hayakufuata kanuni hizo.

Muro amesema, kamati ya Utendaji ya TFF inaonekana imeanzisha kanuni hii ili kuinusuru timu moja pekee ambayo imeshatumia kanuni hiyo.