Thursday , 5th May , 2016

Serikali inapoteza shilingi laki 9 kwa kila tani moja ya mchele inayoingizwa nchini kimagendo jambo linaloathiri uchumi wa nchi na kurudisha nyuma maendeleo ya wakulima wa kilimo cha mpunga ambao kwa mujibu wa takwimu ni wakulima milioni mbili.

Akiongea na East Africa Radio, katika mkutano uliofanywa na Jukwaa Huru la Kilimo kwa kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo nchini, Mkurugenzi wa Baraza la Mchele Tanzania, Winnie Bashagi, amesema uamuzi wa serikali kufuta leseni za uingizwaji wa mchele itaokoa soko la Tanzania kwa zao hilo nje ya nchi.

"Kama bodi ya mchele tunaishukuru serikali kwa kuzuia leseni za kuuza mchele nje ya nchi, kwa sasa tutaongeza juhudi ya uzalishaji wa zao la mchele ili kumudu mahitaji ya soko la ndani na baadae kuuza mchele wetu nje ya nchi," alisema Bashagi.

Naye Mkurugenzi wa Jukwaa Huru la Kilimo ANSAF, Bw. Audax Lukonge, amesema ili serikali iweze kuwanufaisha wakulima wadogo na wakati ni vyema ikapunguza masharti ya mikopo kwa wakulima.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo Tanzania, Robert Pascal, amesema tayari serikali inawakopesha wakulima wa dogo na wakati ili waweze kuzalisha tani 6 kwa hekta moja tofauti na sasa ambapo wanazalisha chini ya tani mbili kwa hekta.

Aidha, zaidi ya wakulima 1,200 tayari wamenufaika na mikopo baada ya kujiunga kwa vikundi ambapo kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 30 zimetumika kutoa mikopo hiyo ambapo, Robert Pascal wa benki ya kilimo amewaka wakulima wote nchini kujiunga kwa makundi ili waweze kupewa mikopo hiyo.