Friday , 28th Oct , 2016

Idadi kubwa ya watu wasio na ajira pamoja na elimu ya ujasiriamali ambayo ingewasaidia kujipatia kipato halali imetajwa kuwa moja ya sasabu zinazochangia ongezeko la vitendo vya uhalifu katika Manispaa ya Kinondoni.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Salum Hapi (kushoto) akishangaa baada ya kupata maelezo ya jinsi mmoja wa wajasiriamali waliowezeshwa kupitia Airtel Fursa anavyoweza kuingiza shilingi laki moja kwa siku kupitia mradi wake wa biashara ndogo ndogo.

 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Ally Salum Hapi, amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam, katika maonesho ya shughuli za wajasiriamali waliowezeshwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kupitia programu ya kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi ya Airtel Fursa.

Katika maelezo yake, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kinondoni amesema ndiyo maana ofisi yake hivi sasa inatekeleza zoezi la utambuzi wa watu wenye nia ya kujihusisha na ujasiriamali ili wawe sehemu ya wanufaika wa shilingi milioni hamsini ambazo Rais Dkt. John Pombe Magufuli amepanga kuzitoa kwa kila kijiji na mtaa nchini.

Katika maonesho hayo, Airtel imewakilishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Bi. Beatrice Singano ambaye amesema Airtel Fursa imeweza kuibua makundi ya Watanzania wenye vipaji ambao baada ya kupatiwa mafunzo na uwezeshaji kutoka kampuni hiyo wameweza kujikomboa kiuchumi.