Wednesday , 2nd Nov , 2016

Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3 katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kukarabati, kupanua na kumalizia ujenzi wa mabweni mapya pamoja na majengo ya utawala katika baadhi ya magereza nchini.

Wazir Mwigulu Nchemba ziarani katika gereza la Mpanda

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amethibitisha hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Bunge Viti Maalum, Mh. Hawa Mwaifunga lililohoji kuhusu mpango wa Serikali kuhakikisha hali ya magereza katika Mkoa wa Tabora zinaboreshwa.

Mh. Mwigulu amesema kuwa Serikali inaendelea na mpango endelevu wa kufanya upanuzi wa magereza ya zamani na kujenga magereza mapya katika kila wilaya ambapo utekelezaji huo unafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.

Ameongeza kuwa serikali inatambua msongamano wa mahabusu uliopo katika magereza mengi nchini na kuongeza kuwa Jukwaa la Haki Jinai limekuwa likifanya vikao vya kuharakisha kesi ambazo upelelezi wake haujakamilika ili kupunguza msongamano huo.

Waziri Mwigulu Nchemba akitoa ufafanuzi bengeni mjini mjini Dodoma

Aidha, amesema, Serikali inahakikisha Askari Wapelelezi wanapewa mafunzo kulingana na kazi yao ili waweze kufanya ukamataji wa watuhumiwa kwa kuzingatia uzito wa ushahidi wa mhusika na kuepusha malalamiko ya kubambikiwa kesi na kujikuta serikali inatumia gharama nyingi kuwatunza mahabusu hao.

Kuhusu usalama wa askari, Waziri Mwigulu amesema kuwa Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi nchini kwa kuwapa vitendea kazi bora na kuwajengea uwezo wa mafunzo askari hao ili waweze kukabiliana na matukio ya uhalifu dhidi ya wanananchi na mali zao pamoja na uvamizi wa vituo vya polisi nchini.

“Hadi kufikia Septemba 2016 Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha 19 kati ya 23 zilizoporwa kutoka kwa askari waliovamiwa wakiwa wakitekeleza majukumu yao hatua inayoonesha jeshi la Polisi linavyofanya kazi kwa umakini” alisema Mwigulu.