Thursday , 3rd Oct , 2019

Kampeni ya Namthamini,  inayoratibiwa na East Africa Television na East Africa Radio yenye lengo la kumuwezesha mtoto wa kike asikose masomo shuleni akiwa katika hedhi, imeendelea kutoa msaada wa taulo za kike (Pedi) kwa shule mbalimbali  nchini ambapo awamu hii imefika Mbeya.

Baadhi ya wanafunzi na walimu mkoani Mbeya

Kampeni hiyo ya Namthamini imezifikia Shule tatu za Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya  ambazo ni Nsenga, Stellafarm pamoja na Maziwa na kuzungumza na mabinti ambao walieleza changamoto zinazowakabili wanapokuwa kwenye hedhi na namna ambavyo taulo za kike zitawasaidia kuondokana na vikwazo wawapo shuleni.

Walimu wa shule zilizonufaika na msaada wa pedi  wameiomba EATV kuendelea kuzisaidia shule hizo, kwani uhitaji bado ni mkubwa.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Elimu Sekondari Jiji la Mbeya, Hope Mariki amesema jumla ya Wanafunzi 379  wa kike kutoka Shule za Nsenga, Stellafarm na Maziwa wamenufaika na taulo hizo za kike.

Ni miaka mitatu sasa tangu East Africa Television na East Africa Radio, zianzishe  kampeni ya Namthamini yenye kauli mbiu isemayo Namthamini Nasimama Naye ambapo imefika katika mikoa mbalimbali nchini.

Kwa mwaka 2019 pekee tayari imefika katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Dodoma, Tabora na Manyara na kugusa zaidi ya wanafunzi 5000.