Monday , 9th Dec , 2019

Baada ya kuwepo kwa sintofahamu kuhusu jina la uwanja wa klabu ya Simba uliopo Bunju jijini Dar es salaam, msemaji Haji Manara ameeleza jina sahihi la uwanja huo ni Mo Simba Arena na sio Simba Mo Arena kama ilivyotangazwa awali.

Kushoto ni Mohammed Dewji na kulia ni Mshindo Msolla

Taarifa ya Simba leo Desemba 9, 2019, imefafanua kuwa jina hilo linabaki kuwa Mo Simba Arena kwani ni maamuzi ya Mkutano mkuu tofauti na Simba Mo Arena ambayo iliamuliwa baada ya mkutano mkuu.

'Kwa kuwa maamuzi yaliyoafikiwa awali na Wanachama ya kuita uwanja wa Bunju jina la MO Simba Arena yalipitishwa na kwa kuwa badiliko la kutanguliza jina la Simba yalifanyika baada ya Mkutano kufungwa na kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba yanayotambua maamuzi ya ndani ya Mkutano Mkuu yataheshimiwa kabla ya Mkutano kufungwa', imeeleza taarifa ya Simba.

Kwa upande Yanga wao wameendelea kukaa kimya juu ya suala la wachezaji wao Lamine Moro, David Moringa na Sydney Urkhob kuvunja mikataba na kuondoka.

Licha ya taarifa hizo kusambaa huku uongozi ukigoma kutoa ufafanuzi, mchezaji Papy Tshishimbi ameonekana kuweka wazi ukweli baada ya kupost picha akiwa na Lamine Moro na kumtakia kila la kheri.